Home » Highlights » Jacqueline Wolper Kutoka Saluni hadi Uigizaji nyota


Jacqueline Wolper Kutoka Saluni hadi Uigizaji nyota

Posted: 10 Oct, 2011

Usemi huu utaweza kuakisi tasnia ya filamu hapa nchini ambayo baadhi ya wasanii wake wanang’ara na kuwa na mafanikio hivi sasa, lakini wakiwa na historia ya kuanza mikikimikiki mbali huku wakipitia mabonde na milima.

Jacqueline Wolper

Baadhi ya wasanii ambao kwa sasa wanang’ara lakini wamepita safari ndefu ni Steven Kanumba ‘Kanumba’, Vicent Kigosi ‘Ray’, Jacob Steven ‘JB’, Yvonne Cherrie ‘Monalisa’, Lucy Komba na wengineo wengi.

Lakini pia wapo walioanza kuibuka ndani ya miaka takribani mitano iliyopita lakini kwa sasa wamekuwa tishio katika fani hiyo, mmojawapo ni msanii Jacqueline Wolper, ambaye karibu miaka minne, amekuwa mwigizaji nyota wa filamu kutokana na kazi zake kukubalika ipasavyo.

Akizungumza katika mahojiano na HABARILEO Jumapili, Jackline ambaye anazungumza taratibu na kwa kituo na kama ni mtu wa kukurupuka unaweza kumdhania kuwa ana maringo, anaeleza nia yake ya kutaka kuwekeza katika fani hiyo ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wasanii wachanga.

“Pamoja na mafanikio niliyoyapata ndani ya miaka minne, nina kiu ya kujidhatiti katika fani hii. Kiu yangu ni kuhakikisha nafungua kampuni kubwa ya kuuza vifaa vinavyotumika katika filamu, usambazaji wa kazi za filamu na kuanzisha kikundi cha sanaa.

“Napenda sana kuwasaidia na kuwainua wasanii chipukizi kama mimi nilivyoinuliwa, na njia pekee ni kuwa na kikundi amchacho ndicho kitakachokuwa chimbuko la kuibua vipaji vya uigizaji,” anasema.

Jacqueline ambaye pia anapendelea kucheza mpira wa pete (netiboli) anasema kwa mwaka mmoja ameweza kutoa filamu zake zipatazo tatu, huku kazi zake zikisimamiwa na Meneja wake Leah Richard. a.k.a Lamata, ambaye pia ndiye mtunzi wa kazi yake.

Kazi hizo ni Candy, Time After Time na By Princes. Mafanikio hayo ya Jacqueline hayakuja hivi hivi bali yalianzia mwaka 2008 kwa mara ya kwanza aliposhirikishwa kwenye filamu ya kwanza na msanii Lucy Komba kwa kupewa nafasi ya kuigiza katika filamu ya ‘Ama Zangu Ama Zao’, kama Katibu Muhtasi.

Anasema kazi nzuri aliyoifanya baada ya kutambuliwa na aliyekuwa jirani yake (Lucy) aliungwa mkono na kuelekezwa vitu vingi na msanii huyo mzoefu na aliyecheza filamu nyingi za ‘Kipenzi Changu’, Surprise, ‘Red Valentine’ na ‘Family Tears’, ambazo ziliteka soko na kumfanya ajulikane.

Baadaye alitunga filamu zake mbili ya ‘Wekeend’ na ‘My Princess’ ambazo zilifanya vizuri sokoni na akapata moyo wa kuwa mwigizaji rasmi. Filamu nyingine alizoigiza ni ‘Utumwa wa Mapenzi’ na ‘All About Love’ iliyotungwa na Jennifer Kiaka ‘Odama’, ambayo anasema aliipenda kutokana na kuvaa vyema uhusika kwa kuwa aliigiza kama mtoto.

“Filamu ya All About Love ndio filamu niliyoigiza na hata nikiiangalia nakubali kazi niliyoifanya, vile vitu nilivyoigiza asilimia kubwa niliigiza vitu vyangu vya kweli,” anasema. Jacqueline pia anasema filamu iliyomsisimua sana tangu awe msanii ni ‘Last Minutes’ ya Leah, ambayo alicheza na Bajomba.

“Naipenda na huwa nairudia kuitazama kwa sababu inaelimisha, kuna siku wakati natoka super market (dukani) kuna mtu mmoja alilia baada ya kukutana na mimi mlangoni alisema niliigiza maisha yake, lakini bahati nilikuwa pamoja na mtunzi (Lamata) alimuelewesha kuwa hakumtungia mtu kisa kile.

“Lakini pia kuna filamu ya Candy ilikuwa na ugumu wake katika kuigiza hasa kutokana na kuvaa uhusika wa mtu mwenye ugonjwa wa akili ‘chizi’. Kwa watu wengine itakuwa ngumu, lakini kwasababu mimi nina kipaji niliweza.

Nafasi ambazo naweza kuvaa uhusika kikamilifu ni pamoja na kuwa chizi na mtu anayeteswa,” anasema. Jacqueline anasema licha ya kujikita kwenye uigizaji filamu kwa miaka michache, amekuwa nyota anayekabiliwa na migogoro mingi, ambayo anadai haipendi kwa vile si tabia yake.

Anasema anapenda kuelewana, kucheka na kila mtu na hata kubadilishana mawazo, lakini anajuta kwa jinsi umaarufu unavyomuingiza katika matatizo na watu mbalimbali na kuwa wengine wamekuwa wakimfikiria visivyo.

“Ndiyo inatokea hivyo na wakati mwingine magazeti huwa yanaandika tu, na ndiyo yamekuwa chanzo kikubwa cha kutukatisha tamaa. Pia wapo wengine wanataka kukusema vibaya hata kama hakufahamu, wengine wanaweza kuamini kuwa mimi nina tabia mbaya lakini bila kujua ukweli wangu, mimi siko hivyo,” anasema.

Msanii huyo ametoa changamoto kwa wasanii wenzake wa filamu, wasiendekeze migogoro kwa vile haina manufaa yoyote badala yake wajidhatiti katika fani ili kuendeleza sanaa hiyo ambayo anasema sasa imekuwa na soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Anapozungumzia tasnia ya filamu hapa nchini, Jacqueline anasema: “Kinachotakiwa hapa ni kwa wazalendo kuwekeza katika fani hii, filamu zetu ziko juu na hata uwezo wetu wa kuigiza uko juu pia, kinachozuia sanaa kuonekana haina maslahi ni ukosefu wa fedha.

Kwa hakika ukitulinganisha sisi na Wanigeria hakika sisi tuko juu, vikwazo vikiondoka mambo yote yatakuwa sawa.” Jacqueline anasema kujitokeza wageni wengi kuwekeza mitaji yao katika filamu, kunamaanisha kuwa ina faida, na anawataka wazawa kuingiza mitaji yao ili kuongeza ushindani wa malipo kwa wasanii na kuondoa unyanyasaji uliokithiri.

“Kampuni zinazojihusisha na masuala ya kutengeneza filamu na kusambaza ni chache na karibu zote zinashikwa na Waasia, tunataka na Watanzania wengine waweke mitaji yao ili tulipwe vizuri na kutuinua sisi wasanii wa filamu,” anasema.

Akizungumzia manufaa aliyopata katika maisha yake tangu awe msanii wa filamu, anasema ukiachia mbali umaarufu alionao kutokana na tasnia hiyo kutoa nafasi kwake kufahamiana na watu wengi, lakini amenufaika kwa vingi ambavyo amedai ni siri yake.

Jacqueline anasema pamoja na unyonyaji wanaofanyiwa katika filamu, anamshukuru Mungu kwa alichopata maishani mwake, ambapo amekiri wasanii wenye majina makubwa angalau wanaambulia kitu kuliko chipukizi.

“Kwa sisi ambao tayari tuna majina makubwa kidogo alhamdulilah, lakini kwa chipukizi ndiko kuna kilio kikubwa sana kama cha hakimiliki kwani imekuwa vigumu kudhibiti na nadhani hili tatizo halitakwisha vizazi na vizazi,” anasema msanii huyo.

Akizungumzia wasanii wenye uwezo mkubwa, Jacqueline anasema kwanza anajipenda yeye mwenyewe kutokana na uwezo wake katika kuuvaa uhusika, halafu Irene Uwoya kutokana na kufanana naye na pia uwezo wake katika uigizaji ambao alisema anaukubali.

Nje ya nchi anasema anampenda msanii nyota wa filamu wa Marekani, Halle Berry kwa alivyo mtulivu katika uigizaji na msafi.

Jacqueline alizaliwa Moshi Mjini mwaka 1988 na alimaliza elimu ya msingi wilayani Mwanga mwaka 2000 katika Shule ya Msingi Mawenzi, na baadaye kusoma shule za sekondari tofauti za Magrath, Ekenywa lakini aliishia kidato cha tano katika shule ya Masai mwaka 2007 na baada ya hapo hakuendelea na masomo ya sekondari kutokana na sababu ambazo hakutaka kuzitaja.

Baadaye alijiunga na Kozi ya Lugha katika Chuo cha ICC Arusha na kwenda kujiunga na Chuo cha USA Contact na kuhitimu Stashahada ya Masoko na Biashara na kuajiriwa na kampuni hiyo kwa muda mfupi kabla ya kuacha na kuanzisha biashara ya saluni.

“Nilianzisha saluni pale Mwenge, ile bomoabomoa ya kwanza ilinikuta na nikaamua kuihamishia Kijitonyama ambako pia niliamua kuifunga baada ya kuchagua kuendelea na fani ya uigizaji,” alisema Jacqueline ambaye anasema bado anafanya biashara ndogondogo hadi sasa.

Jacqueline anamaliza kwa kusema: “ Kufika kwangu hapa nina watu wa kuwashukuru, kwanza ni Lucy Komba, Ray (Vicent Kigosi), Kanumba (Steven Kanumba) na Mtitu Game.

Imeandikwa na Anastazia Anyimike

Source:

https://www.habarileo.co.tz

Reviews / Comments

 
 
 

ABOUT US

BongoCinema.com is a one-stop online shop offering a huge variety of Bongo Movies on DVDs and Videos from Tanzania ...

Read More

HELP CENTRE and FAQ

# How do I make an order? # How long will it take to receive my order? # What Payment Options do I have? # Cancel my order? ...

Read More

Our Products

Action; Adventure; Comedy; Crime; Documentary; Drama; Educational; Family; Fantasy; History; Horror; Musical; Romance; Spiritual...

Read More

Comments /Maoni

John said, "I think I saw one of those bongo movie … you know those movies of the week. ... toa maoni yako kwenye bongo movie...

Read More