Jane's Journey

Home » Casts » Stanley Msungu


Stanley Msungu

Other Name/s: Stanley Msungu 'Seneta'

Actor

Stanley Msungu 'Seneta'

INGAWA filamu ya ‘Second Wife’, aliyoigiza na ‘Ray’ ndio inayoonekana kama iliyomtambulisha kwa mashabiki, ukweli ni kwamba msanii Stanley Msungu, alishaanza kuonyesha makeke yake kitambo kirefu katika fani hiyo ya uigizaji. Msanii huyo anayefahamika kisanii kama ‘Seneta Msungu’, tangu akiwa shuleni alikuwa mahiri katika fani hiyo sambamba na uchezaji wa ngoma na uimbaji na alishauza sura katika michezo kadhaa ya runinga kupitia kituo cvha ITV akiwa na kundi la Amka Sanaa. Miongoni mwa michezo hiyo iliyodhihirisha kipaji cha msanii huyo ambaye pia ni mahiri katika muziki akiwa ameshafyatua nyimbo tatu mpaka sasa ili kutoa albamu kamili ni pamoja na ‘Lulu’, ‘Safina’ na ‘Dunia’.

Mwenyewe alisema michezo hiyo ilimpa uzoefu wa kutosha katika uigizaji na haikuwa ajabu kwake kuamua kujiengua katika kundi hilo na kutumbukia kwenye uigizaji za filamu kazi yake ya awali kabisa ikiwa ni Last Minutes iliyotoka miaka minne iliyopita. “Baada ya kujiona nimeiva na hali ilivyokuwa katika kundi letu, niliamua kujiengua na kujitosa kwenye filamu na kazi ya kwanza kucheza ni Last Minutes kabla ya kufungukiwa neema kwa kucheza filamu zinazokaribia 30 kwa sasa,” alisema. Msungu, aliyetumbukia kwenye uigizaji kutokana na kuvutiwa na Ramsey Noauh wa Nigeria, alisema baada ya Last Minutes, alicheza filamu za Peace of Mind, Devorce, Devil’s Kingdom, Moses, Ndoa Yangu, I Hate My Birthday, The Shell, Shortcut na sasa akitamba na Rude, moja ya kazi binafsi za mwanadada Jenifer Kyaka ‘Odama’.

Mkali huyo, aliyewahi kung’ara katika soka akiichezea timu yake ya shule na zile mtaani, alisema kati ya kazi zote alizocheza, filamu za Moses, Devil’s Kingdom aliyoigiza na marehemu Steven Kanumba na Ramsey Nouah, Rude na Second Wife ndizo kali kwake. Alisema wakati alipoitwa kwenda kucheza filamu ya Devil’s Kingdom alikaribia kuzimia kutokana na kushindwa kuamini kama angeigiza na Ramsey Nouah anayemhusudu mno. “Sio siri Kanumba ni kama alinifanyia ‘surprise’ kwa kunipa taarifa ya ghafla kwenda kuigiza na hata nilipofika na kuonana uso kwa uso na Ramsey sikuamini. Kwa kweli namzimia mno huyu jamaa na anaweza kazi,” alisema. KIFO Msungu, aliyezaliwa mwaka 1979 wilayani Lushoto, mkoani Tanga akiwa mtoto wa kwanza kati ya sita wa familia yao, alisema wakati tukio la kukutana na Ramsey likiwa ni furaha kwake, kwa upande wa huzuni yapo mambo makuu mawili.

Moja alisema kifo cha wazazi wake, na kunusurika kwake kuuwawa kwa risasi katika tukio la uhalifu lililowahi kutokea eneo la Kigamboni. Alisimulia, Msungu alisema alishawishiwa na rafiki zake aliokuwa akiwaonea wivu kwa namna walivyokuwa ‘mambo safi’ na kumueleza kama anaweza aungane nao kusaka fedha bila kujua kama walikuwa wezi. “Siku moja wananiambia niambatane nao kwenda kuvuna fedha na kuibukia TIPPER ambako kabla sijajua kilichoendelea tulijikuta tukivamiwa na kuwekwa chini ya ulinzi na askari wenye silaha. Kwa kweli nilitahayari mno,” alisema. Alisema askari aliyemwelekezea silaha, alimwambia akisogea hatua moja tu, angemlipua risasi, lakini kwa ujasiri na kukata kwake tamaa, alimwambia askari yule kama ni risasi basi ampige ya kichwa ili afe mara moja. “Nilimweleza mie sikuwa mhalifu ila niliwafuata wenzangu bila kujua kama ni wezi, hivyo ni bora aniue kwa kunitwanga risasi ya kichwa badala ya kwingine nikihofia kuwapa tabu wadogo zangu niliokuwa nawatunza,” alisema. Alisema aliyatamka hayo huku akitembea kuelekea baharini akiamini askari yile angemuua, cha ajabu alikuja kuzinduka keshoye akiwa majini alfajiri bila jeraha lolote ilihali mwanzoni aliamini alikuwa amekufa. Alidai tangu tukio hilo, alishika adabu na kuwaepuka rafiki zake hao na kuamua kuhangaika kwa kutumia vipaji vyake vya uigizaji na muziki.

Msungu anayependa kula ugali kwa bamia au wali kwa njegere na kunywa juisi, alisema japo hajanufaika sana na sanaa, lakini anashukuru fani hiyo imemsaidia kwa mengi kimaisha. “Sina cha kujivunia, ila nashukuru sanaa imenisaidia kwa mengi na jinsi fani inavyozidi kukua naamini nitafika mbali kimaisha, na kutimiza ndoto za kuwa mtayarishaji na kumiliki kampuni binafsi ya filamu,” alisema. MUZIKI Msungu, anayezishabikia timu za Yanga, Barcelona na Liverpool, akiwazimikia nyota wa timu hizo, Haruna Niyonzima, Lionel Messi na Luis Suarez, alisema baada ya kutamba kwenye filamu sasa amehamishia makali kwenye muziki.

Alisema mpaka sasa amepakua nyimbo tatu, ya kwanza ikiendelea kutesa kwenye runinga unaoitwa ‘Unanitesa’ alioimba na Milan wa Bana Marquiz, ‘Nalia’ na mapema wiki hii alirekodi kibao kiitwacho ‘Mikosi’. “Lengo langu kabla ya mwisho wa mwaka huu niwe nimeshatoa albamu kamili itakayokuwa na nyimbo nane za miondoko mchanganyiko ya Zouk na Kwaito,” alisema. Alidokeza atakuwa akisambaza video za nyimbo hizo tu kabla ya kutoa ‘audio’ baadae ili kuepuka ‘kuchakachuliwa’ na baadhi ya wajanja wanaiba kazi za wasanii.

Msungu anayewakubali waigizaji kama Sajuki, marehemu Kanumba, Ray, Gabo, Odama, Riyama Ally na Jackline Wolper, alisema ili wasanii wa Tanzania wafike mbali ni lazima wapendane, kushirikiana na kuwa wa moja. “Sio siri wasanii wengi nchini hatupendani na tunaendekeza majungu na unafiki vitu ambavyo sio vizuri kwa maendeleo ya sanaa zetu,” alisema. Alisema, pia ni vema wasanii hasa watayarishaji na waigizaji wa filamu kuwa wabunifu kwa kutunga visa vinavyorandana na mazingira ya Tanzania. “Tubuni kazi zinazoendana na uhalisi wa maisha wa watanzania, pia serikali itusaidie na kuturuhusu kutumia maeneo yatakayoitangaza nchi,” alisema. Alisema wasanii wanapotaka kuigiza katika maeneo yatakayotoa uhalisia wa simulizi la kazi zao, hupata usumbufu na kuchangia kazi nyingi kulipuliwa na kutokuwa na uhalisia wa mambo. Msungu aliyepania kuja kuwasaidia vijana wenye vipaji, alisema kuna haja pia ya serikali kusaidia kukomesha wizi wanaofanyiwa wasanii katika kazi zao, sambamba na kutazama sanaa kama eneo la kupatia pato la taifa. Mkali huyo anayechizishwa na nguo za rangi ya kahawia (brown), hajaoa ila ana watoto wawili ambao mmoja anasoma mjini Morogoro na mwingine Kigamboni anapoishi yeye. Mwisho

Filmography / Discography


External Links

  • Facebook Page of Stanley Msungu
  • Twitter Page of Stanley Msungu
  • YouTube of Stanley Msungu
  • Website of Stanley Msungu
 
 
 
 

ABOUT US

BongoCinema.com is a one-stop online shop offering a huge variety of Bongo Movies on DVDs and Videos from Tanzania ...

Read More

HELP CENTRE and FAQ

# How do I make an order? # How long will it take to receive my order? # What Payment Options do I have? # Cancel my order? ...

Read More

Our Products

Action; Adventure; Comedy; Crime; Documentary; Drama; Educational; Family; Fantasy; History; Horror; Musical; Romance; Spiritual...

Read More

Comments /Maoni

John said, "I think I saw one of those bongo movie … you know those movies of the week. ... toa maoni yako kwenye bongo movie...

Read More