Jane's Journey

Home » Casts » Hussein Mkiety


Hussein Mkiety

Other Name/s: Hussein Mkiety a.k.a Sharo Millionare

Date/s: 12 September 1987 - 26 November 2012

Actor | Commedian | Singer | TV Presenter

Sharo Milionea a.k.a Muuza Sura, Mpaka Poda alizaliwa mwaka 1987 katika kijiji cha Lusanga, Muheza, Tanga. Na kwamba, alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Lusanga na baadaye kujiunga na Sekondari ya Kwabutu alikosoma hadi kidato ya tatu alipoacha shule kutokana na matatizo ya kifamilia.

Hussein Mkiety a.k.a Sharo Millionea

Lakini baada ya kusota kijijini na kuona maisha hayaendi, mwaka 2003 aliamua kulivaa jiji la Dar es Salaam, kuungana na mama yake ambaye alikuwa mjasiriamali mdogo.

“Baada ya kufika Dar nikapelekwa kujifunza masuala ya ufundi magari kwenye gereji moja ambako nilikaa wiki mbili na baadaye nikapelekwa kwenye ufundi wa mafriji (majokofu) ambako nilijifunza kwa wiki tatu, nako huko maisha yalizidi kuwa magumu kwangu, nikaamua kuhamia kwenye biashara ndogo ndogo na nilifikia hata kuuza magazeti kule Kiwalani,” anasema.

Anasema baadaye mama yake aliamua kurejea Muheza kwenda kumuuguza bibi yake na kujikuta akiishi peke yake katika jiji hili la Dar es Salaam.

“Baada ya mama kuondoka, nilibaki mwenyewe, gharama zangu za maisha nilizibeba mwenyewe, kusema ukweli maisha yalikuwa magumu sana kwa upande wangu.”

Msanii huyo anaongeza kusema: “Muonekano wangu uliwafanya watu wengi wanisukume kuingia kwenye fani hiyo akiwamo rafiki yangu Chiba (msanii Siasa Mohammed), kutokana na matendo yangu, lakini wakati huo nilikuwa naimba mwenyewe mitaani.”

Anasema mwaka 2005 akiwa na marafiki zake Snura Mushi, Nas na Dats waliamua kuunda kundi lao la muziki na kuandaa nyimbo kadhaa, lakini kundi hilo halikudumu baada ya Snura kujiengua na kwenda kuigiza filamu ya Jumba la Dhahabu.

Anakumbuka kwamba, naye aliamua kujiunga na kundi la maigizo la Jamal Arts lililokuwa chini ya Gumbo Kihorota na hapo aliweza kuigiza filamu ya Zinduna na Itunyama ambayo aliigiza na wasanii kama Emmanuel Mgaya ‘Masanja’, Alex Chalamila ‘McReagan’, “Mbali na uigizaji, Mungu amenisaidia nina utundu wa utunzi pia, na niliweza kutunga filamu moja niliiita Dakika Moja ambayo hadithi yake ilimvutia Snura ambaye aliamua kuitengeneza na kuigeuza jina kwa kuiita ‘Sekunde Chache’.

Anasema kuwa kwa mara ya kwanza alichukuliwa na Musa Kilali na aliigiza kwenye filamu ya vishekesho ya Mbwembe `Vol 2’ ambaye aliigiza kama ’Brazamen’ aliyeko kijijini ambapo alipewa sehemu tatu, filamu hiyo aliigiza na wasanii kadhaa wakiwamo Kiwewe (Robert Augustino), Masele (Christian Masele).

“Kusema ukweli, pamoja na mimi kuwa mchanga, lakini niliweza kufanya vizuri, hii ilinipa nguvu kwani pamoja na ugeni wangu na kuigiza na wakongwe, lakini niliweza kufanya vizuri.”

Sharo Milionea anasema: “ Kutokana na kufanya vizuri, Kiwewe aliniomba niingizwe kwenye filamu yao ya vichekesho iliyoitwa ‘Vichwa Vitatu’, Matumaini (Tumaini Martin) alikuwa na mashaka na alitaka nisishiriki, kwani aliona kama mtu ambaye ni wa hali fulani hivyo nisingeweza kushiriki ipasavyo, niliweza kumhakikishia dada huyo kwa kufanya vizuri katika filamu hiyo.”

Alisema kuwa alifanikiwa kuigiza filamu za komedi zake mwenyewe ambazo aliziita Sharobaro na Sharo Milionea. Alisema mwaka jana aliingia mkataba wa mwaka mmoja na Khalfan Abdallah anayemiliki Kundi la Bongo Super Stars Comedy ambalo linawashirikisha waigizaji kadhaa akiwamo King Majuto na Masele, pia aliigiza komedi ya Back from New York na Mtoto wa Mama ambaye ndiyo iliyoingiza maneno ya ‘Kamata Mwizi Meen’. Akizungumzia safari ya maisha ya usanii, Sharo Milionea anasema:

Sharomilionea ambaye amekuwa maarufu kutokana na staili yake anayotumia katika kuigiza amesema kupitia muziki amefanikiwa kusafiri nje ya nchi na kufanya maonyesho na kulipwa vizuri, na bado anaendelea kupata miariko kwa ajili ya kufanya muziki pamoja na kuamini kuwa kuna baadhi ya wasanii wa kuchekesha ambao wamefaidika na uchekeshaji na kuweza kupata fedha kwa ajili ya kazi hiyo. Msanii huyo ambaye ana mkataba na Kampuni ya Al- Riyamy Production pamoja na kuigiza pia ni mwanamuziki wa kizazi kipya yaani muziki wa Bongo Fleva.

“ Nimepitia maisha ya aina mbalimbali, mabonde na milima, lakini sasa nimeanza kunyanyuka, kwa sababu mimi sanaa yangu ni tofauti tofauti kama ilivyo ya Will Smith, ambaye anaweza kuigiza komedi, filamu na kuimba pia. Anasema: “ Ninachoshukuru, nimeleta mapinduzi makubwa kwenye tasnia ya filamu hususani katika fani ya ucheshi, watu wengi waliamini ili uchekeshe basi ni lazima mtu avae nguo zilizochanika au awe mchafu au apake masizi usoni, lakini mimi nimeonyesha kuwa unaweza kuchekesha hata ukiwa umependeza.”

Sharo Milionea ambaye ameonekana kuzoeleka kuwenye komedi, lakini sasa ameweza kuubeba uhusika wake vizuri katika filamu inayotamba sasa ya Chumo iliyoongozwa na Jordan River yenye maudhui ya kupambana na ugonjwa wa malaria. Katika filamu hiyo, Sharo Milionea ameigiza kwa jina la Juma akiwa ni kijana masikini na ametokea kumpenda Amina (Jokate Mwegelo), ingawa baba yake Amina, Ali alitaka binti yake kuwa na maisha mazuri, hivyo kutaka aolewe na Yustus (Yusuph Mlela) ambaye alitoka kwenye familia ya kitajiri.

Pia Sharo Milionea `ameuza’ sura katika video ya wimbo wa ‘Sababu ya Ulofa” wa msanii Top C. Akizungumza chanzo cha jina la Sharobaro, anasema: “Nilipewa na mashabiki wangu kutokana na staili yangu ya kibrazameni.

Tangu nikiwa mdogo huko Tanga suala la usafi lilikuwa jadi yangu, hata kama nina nguo mbili basi nitazifua, ili mradi nionekane nadhifu.

“ Nilipoitwa jina hilo kuna studio ilikuwa inaitwa sharobaro, kwangu mimi niliona ni kawaida tu, kama kuna MJ Records, kuna ubaya gani kama nitaitwa MJ au kuna Bongo rank, je nikijiita bongo litakuwa jina la mtu?

Lakini baada ya Bob Junior ambaye anamiliki studio ya Sharobaro Records kusema jina lake nikaona isiwe shida, basi mimi nikajiita Sharo Milionea. Anapozungumzia changamoto za kazi ya sanaa, anasema kuwa fani hiyo imekuwa na majungu na kuoneana wivu huku baadhi yao wakikosa ubunifu.

“Fani kwa bongo, bado, ni majungu ndiyo yanayotawala, mfano mzuri ni pale baadhi ya watu walitaka kufanya kazi na mimi wakati nina mkataba, wanataka nifikishwe kwenye vyombo vya sheria kwa sababu ya Sh 50,000 anayotaka kunilipa, haiwezekani, lakini unasikia maneno anaringa sana, yule tumemlea wenyewe.

Anasema, lakini pia baadhi ya wasanii wanakosa ubunifu na ndio maana watu wamekuwa wakiiga staili mbalimbali za uigizaji. “Mimi huwezi ukaniambie niigize kama Kingwendu, ile ni staili yake, hebu waangalie wasanii wanavyoiga staili yangu ya kibrazameni, na ndio maana sasa nimekuja na swaga ya ‘ooh mama’ na hiyo ikianza kuchuja au watu wakiiga basi nitabadilisha nyingine.”

Anapozungumzia wasanii ambao wanakubali kazi zao, anawataja, Joti na King Majuto, “Hawa ni wasanii ninaowakubali sana kwenye fani ya ucheshi. Joti ana mitindo mingi na ya kwake kwake ni mbunifu sana, pia King Majuto ni msanii ambaye si wa kumfananisha na mtu yeyote.

“Kwa kazi nilizofanya na King Majuto, nimejifunza mambo mengi, ni msanii ambaye anabadilika pamoja na utu uzima wake, kuna komedi tumeigiza naye inaitwa Alosto, ameigiza kama teja, yaani ameweza kuigiza kama teja wa kweli.” Anasema, kama angepata nafasi ya kuigiza na wasanii wa vichekesho wa nje, angependa kuigiza kama wasanii wenye vituko kama Mr Bean, Eddy Murphy na Will Smith, “ Hawa ni wasanii ambao mara nyingine napenda kuangalia kazi zao na kama ningepata nafasi ya kuigiza nao, basi nigefurahi kuigiza na kiu yangu ingekuwa imekamilika.”

Akizungumzia mafanikio, Sharo Milionea ambaye ametoa wimbo uitwao ‘Kamata mwizi meen’ anasema kuwa sanaa hiyo imebadilisha maisha yake ya awali ya kuwa tegemezi na kuwa mtu anayejitegemea kimaisha ingawa kiu yake kubwa ni kuwa muigizaji wa kimataifa na kujipatia fedha za kuwa mfanyabiashara.

Anasema: “ Hakuna siku niliyokuwa na furaha pale nilipopokea simu kutoka kwa sasa mmoja yuko Marekani anasema kuwa mtaa wao watoto wanamuiga kutembea na vile anavyoongea, na mwingine kapiga kutoka Italia, nimefarijika sana kuona hatimaye kazi yangu inatambuliwa na watu walioko nje.

Akizungumzia umaarufu wake katika sanaa, anasema, “ Kusema kweli nikipita mtaani watu wananiangalia na kama nitakutana na watoto, basi najua hapo lazima nifuatwe nyuma, lakini napendwa na watu wengi hususani akina dada ambao wengi wananisumbua sana, lakini mimi nawapotezea.” “Ule ni uigizaji tu, mimi nina mbio sana, hebu jaribu kuniibia uone, lakini kimtindo ndo ile kamata mwizi meen! Kamata mwizi ni swaga tu,” anasema msanii huyo ambaye hakuna shaka kwamba, ni miongoni mwa nyota wa vichekesho walio juu kwa sasa nchini. Je, atafanikiwa kupaa zaidi kimafanikio au ataishia kulewa sifa na kupotea `kimya kimya’? Bila shaka ni jambo la kusubiri na kuona.

Filmography / Discography


External Links

  • Facebook Page of Hussein Mkiety
  • Twitter Page of Hussein Mkiety
  • YouTube of Hussein Mkiety
  • Website of Hussein Mkiety
 

More Photos

 
 
 

ABOUT US

BongoCinema.com is a one-stop online shop offering a huge variety of Bongo Movies on DVDs and Videos from Tanzania ...

Read More

HELP CENTRE and FAQ

# How do I make an order? # How long will it take to receive my order? # What Payment Options do I have? # Cancel my order? ...

Read More

Our Products

Action; Adventure; Comedy; Crime; Documentary; Drama; Educational; Family; Fantasy; History; Horror; Musical; Romance; Spiritual...

Read More

Comments /Maoni

John said, "I think I saw one of those bongo movie … you know those movies of the week. ... toa maoni yako kwenye bongo movie...

Read More